Simba yaua 4-0, watatu kuikosa Dynamos

© Kwa Hisani

KANDANDA Simba yaua 4-0, watatu kuikosa Dynamos

Zahoro Mlanzi • 20:00 - 26.09.2023

Simba imecheza mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujiandaa na mchezo wao wa marudiano dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Timu ya Simba SC, imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Pan African katika mchezo wa kirafiki uliopigwa leo Uwanja wa MO Arena Bunju, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, mabao ya Simba yalifungwa na Saido Ntibazonkiza, Mosses Phiri, Kibu Denis na Andre Onana.

Simba imecheza mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujiandaa na mchezo wao wa marudiano dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Mchezo huo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utapigwa Oktoba Mosi Uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Katika hatua nyingine, Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally, alisema wachezaji wao Aishi Manula, Henock Inonga na Aubin Kramo ndio watakaoukosa mchezo huo wa Jumapili.

"Hadi sasa naweza kuthibitisha ni wachezaji watatu pekee ambao ni Manula, Kramo na Inonga ndio watakaokosekana katika mchezo wetu unaofuata kutokana na kuwa majeruhi, wengine wote wapo fiti," amesema Ally.

Amesema Manula bado hajawa fiti licha ya kufanya mazoezi ya uwanjani na wenzake ila wanatarajia hadi mwishoni mwa mwezi huu anaweza kuanza mazoezi ya golini.

Amesema upande wa Kramo bado hajawa fiti kucheza mechi za ushindani hivyo anaendelea kujitafuta wakati Inonga yeye bado kidonda chake hakijapona vizuri.

Ameendelea kuzungumzia maendeleo ya beki, Che Malone Fondoh ambaye alipata ajali ya gari mwishoni mwa wiki, amesema yupo fiti na anafanya mazoezi kama kawaida.

Tags: