TFF, Saudi Arabia kushirikiana maendeleo ya soka Tanzania

KANDANDA TFF, Saudi Arabia kushirikiana maendeleo ya soka Tanzania

Zahoro Mlanzi • 15:34 - 21.12.2023

Makubaliano ya ushirikiano huo yalifikiwa nchini Saudi Arabia ambapo Rais wa TFF, Walace Karia ndiye aliyesaini mkataba huo

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeingia mkataba wa ushirikiano na Saudi Arabia wa maendeleo ya soka.

Mkataba huo umesainiwa na Rais wa TFF, Wallace Karia sambamba na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Saudi Arabia, Yasser Al Misehal.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, baadhi ya maeneo ya kipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na kuboresha miundombinu, utawala, waamuzi, timu za taifa, soka la wanawake na vijana, ufundi na mpira wa ufukweni.

"Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limeingia mkataba wa ushirikiano na Saudi Arabia ukaosimamia maendeleo ya soka nchini," imesomeka taarifa ya TFF.

Mkataba huo umesainiwa nchini Saudi Arabia ambapo Rais Karia aliambatana na Makamu wake, Athuman Nyamlani wakati wa tukio hilo.

Ikumbukwe kuwa nchi ya Saudi Arabia ni moja kati ya mataifa ambayo yanatajwa kuja juu katika maendeleo ya michezo duniani.

Kwasasa Ligi ya Saudi Arabia, imejitengeneza kuwa inayofuatiliwa zaidi na mashabiki wa soka kutokana na aina ya sajili za kuvutia ambazo zimekuwa zikifanywa na timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Msimu huu tu timu zinazoshiriki ligi hiyo zilifanya kufuru ya usajili kwa kujizolea nyota wakubwa ambao walikuwa wanacheza Ulaya akiwemo Cristiano Ronaldo, Sadio Mane, Karim Benzema, Neymar, Fabinho, Ng'olo Kante na Ruben Neves.