Simba SC yaichapa Mashujaa FC 1-0 Ligi Kuu

Kiungo wa Simba SC, Saido Ntibazonkiza (kulia), akishangilia bao lake na Sadio Kanoute

KANDANDA Simba SC yaichapa Mashujaa FC 1-0 Ligi Kuu

Zahoro Juma • 20:04 - 03.02.2024

Ushindi huo umewaifanya kuwasogelea wapinzani wao timu za Yanga na Azam waliopo nafasi mbili za juu

Wekundu wa mitaa ya Msimbazi, timuya Simba SC, imeanza vyema kampeni yao ya kula viporo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja wa ugenini dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma.

Ushindi huo katika Uwanja wa Lake Tanganyika, umewafanya Simba kufikisha alama 26 na kuwasogelea wapinzani wake wawili waliojuu yake Azam na Yanga.

Bao la ushindi katika mchezo huo, lilifungwa dakika ya 16 kipindi cha kwanza kupitia kwa Saido Ntibanzokiza aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

Simba ilionekana kucheza kwa maelewano kipindi cha kwanza licha ya kuwa Kocha, Abdelhak Benchikha alianzisha wachezaji wawili wapya, Freddy Michael Koublan na Babacar Sarr.

Penalti ya Simba ilipatikana baada ya mlinzi wa Mashujaa, Mpoki Mwakinyuke kumuangusha Kibu Denis ndani ya eneo la hatari.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mashujaa, kubadilika kimchezo na nafasi kubwa ambayo walitengeneza ilikuwa dakika ya 68 ambapo kiungo, Zuber Dabi alipiga kichwa ambacho kiligonga mtamba wa panya baada ya kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Abdulrahman Mussa.

Kwenye mchezo huo, pia Kocha Benchikha alimpa nafasi kiungo wake, Clotus Chama Ikiwa ni siku moja tu baada ya uongozi kumsamehe kutokana na tatizo la utovu wa nidhamu.

Kwa matokeo hayo Simba, inaendelea kusalia katika nafasi ya tatu kwa alama zao 26 huku Mashujaa wakiwa nafasi ya 15 na alama zao 9.

Mara baada ya michezo huo, Simba itashuka tena dimbani Jumanne kucheza dhidi ya Tabora United katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mkoani Tabora.