Simba SC kuivaa Jwaneng Galaxy ikiwa na mambo matatu kichwani

Meneja Habari na Mawasiliano wa timu ya Simba SC, Ahmed Ally, akizungumzia maandalizi hayo

KANDANDA Simba SC kuivaa Jwaneng Galaxy ikiwa na mambo matatu kichwani

Na Zahoro Juma • 22:05 - 26.02.2024

Ni katika mchezo wa kuamua hatma ya timu hiyo kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utapigwa Jumamosi jijini Dar es Salaam

Uongozi wa Klabu ya Simba SC, umetangaza kusaka mambo matatu kuelekea mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao watacheza Machi 2 dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Mchezo huo ni wa kuamua hatima ya Simba katika michuano hiyo msimu huu utachezwa saa 1 usiku katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wamepania kushinda mchezo huo kwa lengo la kufuzu kucheza hatua ya robo fainali.

Mbali na lengo la kufuzu lakini pia wanataka kulipiza kisasi kwa Jweneng ambao msimu wa 2021-22 waliwafunga Simba kwenye Uwanja wa Mkapa kwa jumla ya mabao 3-1 na kuwanyima fursa ya kwenda hatua ya makundi.

Aidha amesema pia kama watafanikiwa kushinda na kutinga hatua ya robo fainali basi kuna rekodi watakuwa wameweka ya kuwa miongoni mwa timu tano ambazo zimefanikiwa kucheza hatua hiyo kwa misimu minne mfululizo.

"Tunaingia katika mchezo huu tukiwa na mambo matatu kichwani, kwanza kuingia robo fainali, pili kulipa kisasi lakini tatu kuweka rekodi kuwa miongoni mwa timu tano Afrika ambazo zimeingia robo fainali mara nne mfululizo," amesema.

Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B ikiwa na alama 6 sawa na Wydad Casablanca. Hata hivyo 'Wekundu wa Msimbazi' wanajivunia faida ya 'head to head' baina yake dhidi ya Wydad kama timu hizo zikilingana alama baada ya mechi za mwisho.

Katika kundi hilo, Asec Mimosa tayari imeshakata tiketi ya robo fainali kama vinara wa kundi baada ya kupata alama moja katika mchezo wake uliopita waliocheza nyumbani dhidi ya Simba.

Katika hatua nyingine, Ally ametangaza viingilio vya mchezo huo ambapo cha chini kitakuwa ni sh. 5,000 kwa wale watakao kata tiketi katika majukwaa ya mzunguko.

Kwa upande wa VIP C ni sh. 10,000, VIP B ni sh. 20,000 na VIP A ni sh. 30,000.

Hata hivyo kabla ya mchezo huo, Simba inatarajiwa kushuka uwanjani Jumatano kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Azam Sports Federation Cup dhidi ya TRA Kilimanjaro.

Tags: