Wapinzani waliopo njiani kukutana na Yanga SC robo fainali CAF

Wachezaji wa timu ya Yanga SC, wakishangilia moja ya bao walilofunga dhidi ya Belouizdad

KANDANDA Wapinzani waliopo njiani kukutana na Yanga SC robo fainali CAF

Na Zahoro Juma • 20:03 - 26.02.2024

Ni baada ya kutinga hatua hiyo kwa kishindo kwa kuitandika CR Belouizdad mabao 4-0

Baada ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu ya Yanga SC, hadi sasa tayari timu tatu zina nafasi kubwa ya kupangwa kucheza na miamba hiyo katika hatua hiyo.

Ushindi wa mabao 4-0, walioupata Yanga mbele ya CR Belouizdad mwishoni mwa wiki, umeiwezesha timu hiyo kutinga robo fainali huku ikiwa na mechi moja mkononi ya kuamua nani ataongoza Kundi D linaloongozwa na Al Ahly.

Droo ya robo fainali ya michuano hiyo inatarajia kupangwa mapema mwezi ujao na mechi zake zitaanza kuchezwa mwishoni mwa mwezi huo.

Yanga kama hawatapata matokeo ya ushindi kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Al Ahly itakayopigwa Ijumaa, itakuwa imemaliza katika kundi hilo kwa kushika nafasi ya pili ambapo kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinazoendesha michuano hiyo, itakuwa na nafasi ya kukutana na washindi wa kwanza katika makundi mengine isipokuwa timu ambayo katoka nayo kundi moja.

Kwa msimamo wa makundi mengine unavyoonekana hadi kufikia mechi hizi za mzunguko wa tano kabla ya kuhitimishwa hatua hiyo, timu ya Asec Mimosa pekee kutoka Kundi B ndiyo imejihakikishia kumaliza kinara wa kundi, hivyo moja kwa moja anakuwa miongoni mwa timu ambazo zinaweza kucheza na Yanga katika hatua ya robo fainali.

Msimamo wa Kundi A unaongozwa na Mamelod Sundowns wa Afrika Kusini yenye alama 10 sawa na TP Mazembe ambao wapo nafasi ya pili. Timu hizo zote mbili zimeshafuzu kutokea kundi hilo lakini wawili hao watakutana nchini Afrika Kusini mwishoni mwa wiki hii ili kuamua nani awe kinara.

Kama msimamo wa kundi utaendelea kusalia kama ulivyo hivi sasa hadi mechi za mwisho zitakapokamilika basi ni wazi mpinzani wa pili kwa Yanga katika droo ya hatua ya makundi atakuwa ni Mamelodi.

Katika Kundi C hadi sasa vinara ni Petro Atletico ya Angola ambao wana alama 9 na wakifuatiwa na Esperance ya Tunisia wenye alama 8.

Petro wao imeshajihakikishia kufuzu katika hatua ya robo fainali na wanakibarua cha nyumbani kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Etoile du Sahel ambapo kama watashinda basi watajihakikishia kuongoza kundi na kuwa miongoni mwa timu ambazo zinaweza kucheza na Yanga.

Tags: