Rupia apiga mbili Singida FG ikishinda 4-1 Mapinduzi Cup

KANDANDA Rupia apiga mbili Singida FG ikishinda 4-1 Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 09:46 - 30.12.2023

Nyota huyo wa kimataifa wa Kenya amekuwa na wakati mgumu ndani ya kikosi hicho lakini huenda akarejesha makali kupitia michuano hiyo

Klabu ya Singida FG, imetoa somo kwenye michuano ya Mapinduzi msimu huu baada ya kuwatandika JKU kwa mabao 4-1 katika michuano ya Mapinduzi Cup.

Singida FG ambao msimu uliopita walifika hadi hatua ya fainali na kufungwa na Mlandege, inakuwa timu ya kwanza kuvuna idadi kubwa ya mabao kwenye michuano ya msimu huu.

Mabao ya Singida FG katika mchezo huo wa Kundi B, yalifungwa na Elvis Rupia raia wa Kenya ambaye alifunga mawili huku mabao mengine yakifungwa na Meddie Kagera na Fancy Kazadi ambaye pia alikuwa mfungaji bora wa msimu uliopita.

Bao la kufutia machozi kwa JKU lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Saleh Masoud.

Katika mchezo huo, Rupia ametajwa kuwa Mchezaji Bora wa mechi na alikabidhiwa kiasi cha Tsh500,000 na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambao ni wadhamini wa tuzo hiyo.

Katika mchezo wa mapema uliochezwa saa 10 alasiri, KVZ walipata ushindi wa mabao 2-0. Mabao ya ushindi katika mchezo huo wa Kundi C yalifungwa na Akram Muhina Omar 'Haaland'.

Jumamosi michuano hiyo itaendelea kwa michezo miwili ambapo Mlandege watacheza na Vital'O katika mechi ya awali na Azam watacheza na Chipukizi katika mechi ya saa mbili usiku.