Rais Yanga kutimua wachezaji wavivu, wazembe

KANDANDA Rais Yanga kutimua wachezaji wavivu, wazembe

Zahoro Mlanzi • 15:31 - 09.01.2024

Kauli hiyo imekuja baada ya timu yake kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Mapinduzi Cup na APR ya Rwanda.

Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, amesema hawatamvumilia mchezaji yeyote ambaye hajitumi pindi anapopewa nafasi ya kucheza uwanjani.

Aidha Hersi amesema wanachama na mashabiki wa Yanga watarajie kuona sura mpya za wachezaji kabla ya dirisha hili la usajili kufungwa huku baadhi ya wachezaji watapewa mkono wa kwaheri.

Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala mbalimbali ya klabu hiyo.

Akijibu swali kuhusu ushiriki wa Yanga katika michuano ya Mapinduzi Cup, Hersi, amesema maamuzi na mikakati yote ya timu huwa wanamuachia kocha na yeye ndio anaamua kitu gani anahitaji.

Amesema kwenye michuano ya mwaka huu Kocha, Migeul Gamondi, aliamua kutumia wachezaji vijana na wale ambao hawakuwa na nafasi ya mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza lengo ikiwa ni kukifanyia tathmini kikosi chake.

"Kocha ndio huwa anaamua anataka kuona nini kwenye michuano ya Mapinduzi, kwahiyo sisi huwa ni watekelezaji tu wa mipango yake," amesema.

Amesema tathimini na muelekeo wa kikosi cha kwanza huwa wanaifanya pia kupitia michuano ya Mapinduzi na kama mchezaji haoneshi jitihada basi huwa hawana budi kufanya maamuzi ya kumuweka pembeni.

Yanga wameondoshwa katika michuano hiyo katika hatua ya robo fainali baada ya kufungwa 3-1 na APR kutoka Rwanda.

Wakati huo huo, Hersi amesema wao kama uongozi wamefurahishwa na ushiriki wa vijana katika kikosi cha kwanza na kwamba wataendelea kufuatilia maendeleo yao kwa karibu ili waje kuisaidia timu kwa kipindi kirefu kijacho.

Kikosi cha Yanga tayari kimerejea Dar es Salaam kikitokea Zanzibar ambapo wachezaji wanatarajia kuwa na siku kadhaa za mazoezi kabla ya kurejea tena mazoezini kujiwinda na michezo ya mashindano mbalimbali iliyosalia.