Beki wa Simba ashonwa nyuzi 13 mguuni

© Kwa Hisani

KANDANDA Beki wa Simba ashonwa nyuzi 13 mguuni

Festus Chuma • Zahoro Mlanzi • 18:00 - 22.09.2023

Beki wa Simba SC, Henock Inonga, amechanika kidogo mguuni baada ya kuchezewa rafu, lakini anaendelea vizuri na ameruhusiwa kurudi nyumbani.

Beki wa timu ya Simba SC, Mkongo Henock Inonga, ameshonwa nyuzi 13 baada ya kuchezewa rafu mbaya mguuni na winga wa Coastal Union ya Tanga, Haji Ugando.

Inonga alifanyiwa faulo hiyo dakika ya 19 iliyosababisha Ugando kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na Mwamuzi, Ahmed Arajiga wakati Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Hata hivyo mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Beki huyo kisiki, alitolewa uwanjani kwa machela baada ya kushindwa kutembea na moja kwa moja kupakiwa ndani ya gari la wagonjwa mahututi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Daktari wa timu hiyo, Edwin Kagabo, beki huyo amechanika kidogo juu ya kifundo cha mguu na ameshonwa nyuzi 13 lakini anaendelea vizuri na ameruhusiwa kurudi nyumbani.

"Inonga amesharuhusiwa na yupo nyumbani, amepata jeraha pale pale alipoumia wakati wa mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, jambo zuri ni kuwa hajavunjika mfupa ni kidonda tu," amesema Kagabo.

Kuhusu atakuwa nje ya Uwanja kwa muda gani, Dkt. Kagabo amesema itategemea na jinsi kidonda kitakavyopona lakini haikuwa rafu mbaya sana.

Simba itashuka uwanjani Oktoba Mosi kurudiana na Power Dynamos ya Zambia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezo wa awali timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Tags: