Zayd aongeza miaka miwili kubakia Azam FC

© Kwa Hisani

KANDANDA Zayd aongeza miaka miwili kubakia Azam FC

Zahoro Mlanzi • 12:32 - 31.10.2023

Mkataba wake wa awali ulikuwa unatarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu huu, hivyo sasa mkataba wake mpya utamuhakikishia maisha marefu zaidi na miamba hiyo.

Kiungo mshambuliaji wa timu ya Azam FC, Yahya Zayd, ameongeza mkataba wa miaka miwili ambao utamuweka kwenye viunga vya Chamazi Complex hadi mwaka 2026.

Mkataba wake wa awali ulikuwa unatarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu huu, hivyo sasa mkataba wake mpya utamuhakikishia maisha marefu zaidi na miamba hiyo.

Mchezaji huyo ambaye hakuonekana uwanjani kwa siku za hivi karibuni ni zao la Azam na ameitumikia timu hiyo kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa kijamii wa timu hiyo, saa chache kabla ya kikosi cha Azam kusafiri kwenda Kigoma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Mashujaa FC, ilionesha kiungo huyo akisaini mkataba huo.

Mchezo dhidi ya Mashujaa ni wa mzunguko wa nane, unatarajiwa kuchezwa Jumatano kwenye uwanja wa Lake Tanganyika.

Timu zote zinaingia kwenye mchezo huo zikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutoka kupoteza mechi zao zilizopita.

Mashujaa wao mara ya mwisho kushuka dimbani ilikuwa ni Oktoba 25 ambapo walialikwa na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani na wakikubali kichapo cha 2-0.

Kwasasa wapo nafasi ya 6 wakiwa na alama 8 baada ya kushuka dimbani mara sita huku mechi yao moja dhidi ya Simba ikiwa imehairishwa.

Kwa upande wao, Azam wametoka kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Yanga na Namungo hivyo wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na majeraha makubwa.