Simba SC yaitia presha Yanga SC kileleni

Kiungo wa Simba, Clatosu Chama (kushoto), akitafuta njia ya kumtoka Matteo Anthony wa JKT

KANDANDA Simba SC yaitia presha Yanga SC kileleni

Na Zahoro Juma • 19:43 - 15.02.2024

Ni baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kutofautiana na Yanga kwa alama 4

Bao pekee lililofungwa na Kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama, limeiwezesha timu ya Simba SC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, limeifanya Simba kufikisha alama 36 nyuma ya Yanga inayoongoza ligi hiyo ikiwa na alama 40.

Timu hizo ambazo ni mahasimu wa kubwa wa soka la Tanzania, zimemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, zikitofautiana kwa alama 4 pekee.

Chama alifunga bao hilo dakika ya 33 akiwa nje ya 18 ambapo alipiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni huku Kipa, Yakub Seleman akiruka bila mafanikio baada ya kupokea pasi ya Mohamed Hussein.

Pamoja na Simba kuondoka na ushindi huo, mashabiki wao hawatosita kumpongeza Kipa wao, Ayoub Lakred ambaye aliokoa mabao ya wazi akiwa ana kwa ana na washambuliaji wa JKT.

Straika wa JKT, Sixtus Sabilo alipoteza nafasi mbili za wazi kipindi cha kwanza akiwa ana kwa ana na Lakerd na hata Ismail Kader pia alikosa bao la wazi ambapo kipa huyo aliokoa mashuti yao kwa kutumia miguu.

Uwanja huo umefunguliwa kwa mara ya kwanza kuchezewa katika mechi za ligi hiyo huku ukarabati ya majukwaa ukiwa unaendelea kitu ambacho kiliwanyima fursa mashabiki kujitokeza kwa wingi.

Katika mchezo huo, JKT ilionesha kandanda safi tofauti na ilivyotarajiwa na wadau wengi wa soka kutokana na muda mwingi kushambulia lango la Simba na si kukaa nyuma ya mpira.

Matokeo hayo, yameifanya JKT Tanzania kubaki katika nafasi yao ya 13 kwa kuwa na alama 16 huku ikiwa juu ya Tabora United, Mashujaa FC na Mtibwa Sugar.