Siku 10 za moto kwa Simba SC na Yanga SC

Wachezaji wa timu ya Simba SC, wakiwa mazoezini

KANDANDA Siku 10 za moto kwa Simba SC na Yanga SC

Zahoro Juma • 21:20 - 29.01.2024

Ni baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuzipangia kucheza mechi saba

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, imepanga ratiba ya mechi za viporo vya mzunguko wa kwanza ambapo ndani ya siku 10 timu ya Simba SC zinatakiwa kucheza mechi nne huku Yanga wakicheza mechi zao tatu.

Ratiba hiyo inatarajia kuanza Februari 2 ambapo Yanga itakuwa ugenini mkoani Kagera kucheza dhidi ya Kagera Sugar huku watani zao Simba wakishuka dimbani siku inayofuata kucheza dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika.

Katika michezo yao mitatu, Yanga mara baada ya kutoka Kagera watacheza mechi mbili nyumbani ambazo ni Februari 5 dhidi ya Dodoma FC na Februari 8 dhidi ya Mashujaa.

Kwa upande wa Simba, wao watacheza michezo mitatu ugenini kuanzia hiyo mechi ya Mashujaa. Mechi nyingine za ugenini ni Februari 6 dhidi ya Tabora United na Februari 12 dhidi ya Geita Gold.

Mechi pekee ambayo Simba itakuwa nyumbani ni dhidi ya Azam FC ambapo imepangwa kuchezwa Februari 9.

Hata hivyo mechi hiyo bado haijapangiwa uwanja kutokana na wenyeji hao kutotaja uwanja mbadala baada ya Uhuru na Mkapa kufungiwa kwa muda.

Inaelezwa uongozi wa Simba upo katika harakati za kutaka kuutumia Uwanja wa New Amani Complex, Zanzibar kwa ajili ya michezo yake ya kimataifa huku Sheikh Amri Abeid jijini Arusha watautumia kwa mechi za michezo ya ndani

Mara baada ya kuisha kwa mechi hizo za viporo, ratiba inaonesha mechi za mzunguko wa 15 kwa timu zote zitaanza kuchezwa Februari 11 na kutamatika Februari 16.

Baadhi ya mechi za mzunguko wa 16 ambao ni mzunguko wa pili zitaanza kutimua vumbi kuanzia Februari 15 kwa zile timu ambazo zilianza kucheza mapema kuanzia Februari 11.

Tags: