Nyota watano wanaocheza nje waitwa Twiga Stars

KANDANDA Nyota watano wanaocheza nje waitwa Twiga Stars

Zahoro Mlanzi • 21:03 - 18.11.2023

Baadhi ya nyota hao ni Opa Clement wa Besiktas ya Uturuki na Aisha Masaka wa BK Hancken ya Sweden.

Wachezaji watano wanaocheza timu mbalimbali barani Ulaya, Amerika na Asia, wameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars' kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwakani nchini Morocco.

Twiga Stars inatarajia kuumana na Togo katika raundi ya pili ya michuano hiyo, mchezo utakaopigwa Jumatano ijayo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), timu hiyo itaingia kambini Novemba 22.

Taarifa hiyo imewataja nyota hao wanaocheza nje ya nchi kuwa ni beki Julieath Singano anayecheza Juarez ya Morocco, viungo Enekia Kasonga wa Eastern Flames ya Saudi Arabia na Diana Lucas wa Ameds FK ya Uturuki.

Pia wapo washambuliaji, Opa Clement wa Besiktas ya Uturuki na Aisha Masaka wa BK Hancken ya Sweden.

Kikosi hicho cha Kocha, Bakari Shime, kinaundwa na wachezaji wengi nyota wa timu ya JKT Queens ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake na Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na wawili wa Simba Queens na mmoja wa Yanga Princess.

Baada ya mchezo huo, utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, tiimu hizo zitarudiana mapema Desemba Uwanja wa Kegue jijini Lome na mshindi wa jumla atafuzu kwa fainali hizo.

Tags: