Kocha Mexime aahidi makubwa Ihefu FC

LIGI KUU Kocha Mexime aahidi makubwa Ihefu FC

Na Zahoro Mlanzi • 18:00 - 28.12.2023

Mexime amepata nafasi hiyo ikiwa imepita wiki moja tangu atimuliwe kuinoa Kagera Sugar

Kocha mpya wa kikosi cha Ihefu FC ya mkoani Mbeya, Mecky Mexime, ameahidi kufanya vyema ndani ya kikosi hicho kwa madai kuwa uongozi wa timu hiyo una malengo makubwa.

Hayo amesema muda mfupi tu baada ya uongozi wa Ihefu kumtangaza kuwa kocha mkuu akirithi mikoba ya Mganda, Moses Basena ambaye aliondoshwa katika nafasi yake mwanzoni mwa mwezi huu.

Mexime anaingia katika timu hiyo ikiwa ni wiki moja tu imepita tangu na yeye alipotimuliwa kukinoa kikosi cha Kagera Sugar ambacho kilitoka kupokea vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Simba SC na Azam FC.

Akizungumza na Pulse Sports, Mexime amesema Ihefu ni timu nzuri na yenye malengo makubwa hivyo atajitahidi kuendana na kasi ya uongozi ili kutimiza yale ambayo wamekubaliana.

"Kila timu ina malengo yake kwahiyo kutofanya vizuri sehemu moja haina maana pia utashindwa sehemu nyingine, nimeongea na viongozi wa timu hii wamenihakikishia ushirikiano katika matakwa yangu na mimi naahidi kazi nzuri," amesema Mexime.

Ihefu msimu huu imenolewa na walimu watatu tofauti kuanzia Zuber Katwila akaja Basena na sasa Mexime.

Hadi sasa Ihefu FC imecheza mechi 14 na imekusanya alama 13 wakiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.