TFF yasaini mkataba wa sh bilioni 3 na Sandaland jezi timu za Taifa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeingia mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya sh. bilioni 3 na Kampuni ya Sandaland Fashion Wear kwa ajili ya kuzivalisha timu za taifa.
Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam, mbele ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais wa TFF, Wallace Karia, ameshukuru kampuni hiyo kwani imekuwa ni mkataba wa kihistoria kuwahi kufanyika ndani ya shirikisho hilo.
"Mkataba huu utatupa jezi bure pamoja na fedha taslimu kila mwaka, tumekuwa tukitoa fedha zetu kununulia jezi lakini mkataba huu wa miaka mitano utakaokuwa na thamani ya sh. bilioli 3 utatusaidia sana," amesema Karia.
Amesema kila mwaka watapokea fedha na jezi ambazo watakuwa wakizitumia katika mashindano mbalimbali ndani ya muda huo.
Kwa upande wa Waziri Ndumbaro, ameipongeza TFF kwa kukubali kusaini mkataba huo kwani ni mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania kufanyika.
"Ni mkataba ambao timu zetu zote za Taifa zitakuwa zinatengenezewa jezi na kampuni hiyo, unaweza kuona ni jambo dogo lakini halijawahi kufanyika na linafanyika chini ya Rais Karia," amesema Ndumbaro.
Awali Mmoja wa Waurugenzi wa hiyo, Yusuph Yenga, ameihakikishia TFF watatengeneza jezi zenye ubora wa kiwango cha juu ambazo zitavaliwa na shabiki yeyote.
"Watanzania sisi ni wazalendo na ndio maana tukaona tujitose katika nyanja za kimataifa, sote ni wamoja na sote tutazipendezesha timu zetu za taifa," amesema Yenga.
Baada ya kusainiwa mkataba huo, wadau wa soka, wametoa wameupokea kwa hisia tofauti kwa kila mmoja kutoa maoni yake.
"Ni jambo zuri na la kupongezwa, ni kitu ambacho hakijawahi kufanyika kwa TFF na hii itakuwa imefungua milango kwa kampuni zingine kuchangamkia fursa hiyo pindi mkataba utakapomalizika," amesema Hans Raphael ambaye ni Mchambuzi wa Soka nchini kutoka Wasafi Media.
Pia Jemedari Said ambaye ni Mchambuzi wa Soka kutoka EFM Redio, amesema hiyo kampuni kama imejilipua kwani uuzaji wa jezi za timu ya taifa ni mgumu ukilinganisha na katika jezi za klabu.
"Sijui amefanya uchunguzi kiasi gani lakini naona kama amefanya haraka, uvaaji wa jezi ya taifa mitaani si sana ukilinganisha na jezi za Simba au Yanga," amesisitiza Jemedari.