Timu ya JKT Queens ya Tanzania, imenusa kucheza hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Wanawake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Athletico Abidjan uwanjani Korhogo, Ivory Coast.
Ushindi huo, umeifanya JKT Queens kushika nafasi ya pili ikiwa na alama 3 nyuma ya vinara Mamelodi Sundows Ladies yenye alama 6 huku Athletico na Sporting Casablanca zikiwa na alama 1 kila mmoja.
Wakati Mamelodi ikiwa ishatinga nusu fainali, kazi ipo kwa JKT Queens ambayo ili kujihakikishia kutinga hatua hiyo inatakiwa ishinde mchezo wao wa mwisho bila kuangalia matokeo ya timu zingine.
Mechi inayofuata kwa wawakilishi hao wa Ukanda wa CECAFA ni dhidi ya Sporting Casablanca itakayochezwa Jumamosi kuanzia saa 5 usiku huku Mamelodi ikicheza na Atletico.
Mabao ya JKT Queens katika mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo, yalifungwa na Winfrida Gerald na Alia Salum huku la Atletico likifungwa na Sandrine Niamien.
Baada ya mchezo kumalizika, Kochwa JKT Queens, Ester Chabruma, ameshukuru kumaliza mechi salama na kupata matokeo mazuri.
"Mechi ya kwanza tulipoteza kwakuwa hatukuwa na uzoefu lakini tukaenda katika uwanja wa mazoezi na kufanyia kazi changamoto zetu na ndio maana mechi hii tumepata matokeo," amesema Chabruma.
Amesema walirekebisha makosa waliyoyaona na kuamua kuja kivingine na hatimaye wamepata matokeo mazuri.
Katika mchezo wa awali wa Kundi hilo A, Mamelodi Sundowns, imetinga nusu fainali baada ya kuichapa Casablanca bao 1-0, hivyo kufikisha alama 6.
Bao hilo pekee lilifungwa na Melinda Kgadiete kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Lebohang Ramalepe.