Yanga SC kutumia 'wakaa benchi' Mapinduzi Cup

KANDANDA Yanga SC kutumia 'wakaa benchi' Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 15:00 - 27.12.2023

Baadhi ya wachezaji ambao hawachezi mara kwa mara ni Gift Fred, Zawadi Mauya, Jonas Mkude, Denis Nkane, Aboutwalib Mshery na Crispin Ngushi

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema atatumia wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi chake wakati wa michuano ya Mapinduzi Cup.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kesho kwa kuchezwa mechi mbili ambapo bingwa mtetezi, timu ya Mlandege FC itaumana na Azam FC ikifuatiwa na mechi ya Vital'O ya Burundi dhidi ya Chipukizi United.

Baadhi ya wachezaji ambao hawachezi mara kwa mara ni Gift Fred, Zawadi Mauya, Jonas Mkude, Denis Nkane, Aboutwalib Mshery na Crispin Ngushi.

Akizungumza na Pulsesports kuelekea michuano hiyo, Gamondi, amesema ni michuano mizuri kwani itasaidia kuangalia viwango vya wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza.

"Kwetu itatusaidia ukizingatia ni kipindi cha usajili hivyo tunataka kukitumia vizuri kwa kuangalia wachezaji tulionao kwa kuwapa nafasi nyingine tujiridhishe kama tunaweza kuendelea nao au tutafute wengine," amesema Gamondi.

Amesema wapo wachezaji wengi wanaonekana kuwa na viwango vizuri lakini muda wa kucheza ndio tatizo ila kupitia mashindano hayo wana imani watajua la kufanya.

Katika michuano hiyo, Yanga imepangwa Kundi C pamoja na timu za Jamhuri FC na KVZ zote za Zanzibar huku Jamus FC ikitoka Sudan Kusini.

Makundi mengine ni A lenye timu za Azam FC, Vital'O ya Burundi, Chipukizi na Mlandege zote za Zanzibar wakati Kundi B ni Simba SC, APR ya Rwanda, Singida FG na JKU ya Zanzibar.

Timu za Bandari ya Kenya na URA ya Uganda zimejitoa katika mashindano hayo kutokana na kubanwa na ratiba za ligi za nyumbani kwao.

Bingwa wa michuano hiyo, atazawadiliwa sh. milioni 100 na wa pili atajinyakulia sh. milioni 80.

Tags: