Benchikha 'meno nje' kupata alama moja kwa Asec Mimosa

Kocha wa Simba SC, Benchikha, akiwapongeza wachezaji wake

KANDANDA Benchikha 'meno nje' kupata alama moja kwa Asec Mimosa

Na Zahoro Juma • 16:10 - 24.02.2024

Kocha huyo wa Simba, amefurahia alama hiyo akiamini mechi ya mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy watapata matokeo mazuri

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha, amesema anajivunia kupata alama moja ugenini kwani sio rahisi kucheza dhidi ya Asec Mimosa.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu yake dhidi ya Asec ulioisha kwa suluhu, Benchikha amesema alama moja ni muhimu kwao na sasa akili zao watazihamishia kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy.

"Mechi ilikuwa ngumu hasa ukizingatia ubora wa Asec Mimosa wanapokuwa nyumbani, najivunia wachezaji wangu wamepambana na kupata alama moja ambayo itatusaidia mbele," amesema.

Matokeo ya suluhu yanaendelea kuwabakisha Simba katika nafasi ya pili wakiwa na alama sita nyuma ya vinara Asec Mimosa wenye alama 11 na wakiwa tayari wamefuzu na kujihakikishia kuongoza Kundi B.

Leo katika kundi hilo utachezwa mchezo mmoja kati ambapo Jwaneng Galaxy watakuwa nyumbani wakiwakaribisha Wydad Casablanca na kama wenyeji watashinda basi watafikisha alama saba ambazo zitawapandisha hadi nafasi ya pili.

Ratiba ya mechi za mwisho ambazo zitachezwa Machi 2, Simba watakua nyumbani kuwaalika Galaxy huku Wydad wakiwa nyumbani kucheza na Asec.