Benchikha aahidi makubwa marudiano na Wydad

KANDANDA Benchikha aahidi makubwa marudiano na Wydad

Na Zahoro Mlanzi • 08:00 - 11.12.2023

Kocha huyo wa Simba, amepoteza mechi yake ya kwanza tangu akabidhiwe mikoba kuinoa timu hiyo wiki iliyopita

Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema watajipanga zaidi kupata alama tatu katika mchezo unaokuja wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ambao utapigwa Desemba 19 Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Benchikha ametoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo baina ya timu hizo uliofanyika kwenye Mji wa Marakech nchini Morocco ambapo Simba ilifungwa bao 1-0.

Mchezo huo ulikuwa muhimu kwa timu zote mbili ambazo zilikuwa zinafuatana katika nafasi ya tatu na ya nne kwenye msimamo wa Kundi D.

Kwa ushindi huo, Wydad ambao ilikuwa inaburuza mkia kabla ya mchezo huo, imepanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na alama 3 na kupunguza presha kwa Kocha wao, Adel Ramzi huku Simba wakishuka hadi mkiani baada ya kusalia na alama zao 2.

‘Tumepoteza mchezo muhimu lakini bado nafasi tunayo, mechi inayokuja wiki ijayo itakuwa ni muhimu kwetu kupata ushindi ili tuanze kujiweka vizuri," amesema Benchikha.

Benchikha amekiri kuchukizwa na aina ya bao ambalo walifungwa kwenye mpira wa kutenga dakika za majeruhi lakini aliahidi kurekebisha upungufu uliojikoteza kabla ya kurudiana na wababe hao.

Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Benchikha ambaye aliichukuwa timu hiyo hivi karibuni akirithi mikoba ya Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' aliyetimuliwa Novemba 7.

Katika mchezo wa marudiano baina ya timu hizo, Simba inatarajia kukosa huduma ya kiungo raia wa Mali, Saido Kanoute ambaye amesimamishwa kutokana na kupata kadi tatu za njano katika michezo tofauti kama ilivyo kwa nahodha wa Wydad, Yahya Jebrane.

Kabla ya kukutana na Wydad, timu ya Simba kwanza itacheza mchezo wa Ligi Kuu Desemba 15 ambapo watawakaribisha Kagera Sugar katika mechi yao ya tisa msimu huu.

Tags: