Azam FC yaishusha Yanga SC kileleni

LIGI KUU Azam FC yaishusha Yanga SC kileleni

Zahoro Mlanzi • 11:13 - 08.12.2023

Timu hiyo umepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Tanzania Bara baada ya kuifunga KMC mabao 5-0

Timu ya Soka ya Azam FC, imekaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuichapa KMC mabao 5-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo, umeifanya Azam kufikisha alama 25 na kuishusha Yanga kileleni iliyokuwa na alama 24 huku Simba ikiwa ya tatu kwa alama 19.

Hata hivyo, Azam ipo mbele kwa mechi mbili zaidi ukilinganisha na timu za Yanga na Simba ambazo zimesimama kucheza kutokana na majukumu ya michezo yao ya kimataifa.

Katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja, mabao ya Azam, yalifungwa na Prince Dube aliyefunga mawili, Feisal Salum 'Fei Toto', Gibril Sillar na Ismail Gumbo aliyejifunga.

Hicho ni kipigo cha pili kikubwa kwa KMC kufungwa msimu huu baada ya kupokea kichapo kama hicho kutoka kwa Yanga.

Kwa upande wa Azam, inaonekana timu yao kuendelea kuimarika kwani katika mechi nne za mwisho imefunga mabao 16 kitu ambacho si cha kawaida.

Kabla ya mchezo huo, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, ikashinda 3-1 na Ihefu FC na kisha kuifunga Mashujaa FC 3-0.

Baada ya mchezo huo, Azam itashuka uwanjani Desemba 11 kuumana na JKT Tanzania katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.