Mwakinyo atoa siku 14 Kiduku atafute wadhamini wazichape

NGUMI Mwakinyo atoa siku 14 Kiduku atafute wadhamini wazichape

Na Zahoro Juma • 21:22 - 31.01.2024

Kauli hiyo imekuja baada ya mabondia hao wanaofanya vizuri kwa sasa Tanzania kuwa na malumbano ya muda mrefu mtandaoni

Bondia wa Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania na bingwa wa WBO Afrika, Hassan Mwakinyo, ametoa siku 14 kwa bondia mwenzake, Twaha Kiduku ili kukamilisha utaratibu wa wawili hao kuoneshana ubabe ulingoni.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya vijembe vinavyoendelea kwenye mitandao ya kijamii baina ya mabondia hao ambao wanafanya vizuri kwasasa nchini.

Mwezi uliopita akiwa Zanzibar, Mwakinyo amenukuliwa na vyombo vya habari akitoa kauli ambazo zilitafsiriwa kumlenga Kiduku ambaye kwa muda mrefu wamekuwa wakihusishwa kuwa ni wapinzani.

Kauli hiyo ya Mwakinyo ilikuwa ikikanusha kuwa anaogopa kupigana na mabondia wa Tanzania hasa Kiduku.

"Mimi siogopi kupigana na bondia yoyote wa Tanzania, kwakuwa wamekuwa wakinihitaji kwa muda mrefu sasa nasema nipo tayari kama kuna mtu anataka basi mikataba iwekwe tusaini," amesema.

Hali hiyo ilimfanya kumuibua Kiduku ambaye naye alijibu kuwa yupo tayari kupigana na Mwakinyo ambaye alidai kuwa alikuwa akimkimbia muda mefu.

Kauli ya kuambiwa kuwa anamkimbia Kiduku ndiyo iliyomfanya Mwakinyo kuibuka tena na kutoa siku 14 kwa waandaaji wa mapambano kuandaa pambano hilo ili ubishi umalizwe.

"Ninafanya hili pambano kwa ajili ya mashabiki, naomba hakikisha unaongea vizuri na timu yako ndani ya wiki mbili kabla sijasaini mkataba wa kutetea ubingwa wangu," ameandika Mwakinyo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Tags: