Bondia Mwakinyo kuzichapa na Mzimbabwe Januari 27

NGUMI Bondia Mwakinyo kuzichapa na Mzimbabwe Januari 27

Na Zahoro Mlanzi • 18:21 - 02.01.2024

Hilo litakuwa ni pambano la kuwania ubingwa wa mkanda wa WBO na litakuwa ni la kwanza kwa bondia huyo tangu alipopanda ulingoni mara ya mwisho Aprili, mwaka jana

Bondia wa Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo, anatarajia kupanda ulingoni Januari 27 kuzichapa dhidi ya Enock Msambudzi kutoka Zimbabwe katika pambano ambalo litafanyika katika Uwanja wa Ndani wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Pambano hilo limeandaliwa na Kampuni ya Peak Time Media huku likiwa limepewa idhini na Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Zanzibar (ZPBRC), linatarajia kuwa ni la ubingwa wa WBO.

Hili litakuwa ni pambano la kwanza kwa Mwakinyo tangu lilipotokea sakata lake la kugoma kupanda ulingoni Septemba, mwaka jana kuzichapa na Julius Indongo na kisha kufungiwa kabla ya kufunguliwa mwezi uliopita na TPBRC.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwakinyo amewashukuru waandaji wa pambano hilo kwa kuwa ni pambano zuri na limekuja wakati sahihi wa yeye kuonesha ubora wake katika mchezo wa masumbwi.

"Niseme tu pambano hili limekuja kwa wakati sahihi, nipo tayari kwa ajili ya kupanda ulingoni, nawashukuru waandaaji," amesema.

Mara ya mwisho Mwakinyo kupanda ulingoni ilikuwa Aprili, mwaka jana ambapo alipigana Dodoma dhidi ya Mardochee Kuvesa Katembo.

Kwa upande wa mpinzani wake ambaye ni raia wa Zimbabwe, yeye amecheza mapambano 12 na kushinda 10 huku akipoteza katika mapambano yake mawili mfululizo yaliyopita.

Tags: