Bondia Hassan Mwakinyo arusha kijembe kwa mwenzake Twaha Kiduku baada ya ushindi wake

NDONDI Bondia Hassan Mwakinyo arusha kijembe kwa mwenzake Twaha Kiduku baada ya ushindi wake

Na Zahoro Mlanzi • 19:36 - 27.12.2023

Ushindi huo umepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki na wadau wa ngumi nchini Tanzania kutokana na kiwango cha Kiduku alichokionesha

Bondia wa Ngumi za Kulipwa Tanzania, Hassan Mwakinyo, amerusha kijembe kwa bondia mwenzake, Twaha Kiduku ambaye usiku wa kuamkia jana alipata ushindi wa 'mbinde' dhidi ya Mohamed Sebyala kutoka Uganda.

Kiduku ameshinda kwa pointi mbele ya Sebyala katika pambano la raundi 10 la ubingwa wa PST ambalo lilifanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Hata hivyo licha ya kuibuka na ushindi huo lakini maoni yamekuwa ni mengi kwenye mitandao ya kijamii hasa kuhusu uwezo ambao alionesha Kiduku kwenye pambano hilo huku wengi wakiamini hakikuwa kiwango kizuri.

Jambo hilo pia ndio lililomuibua Mwakinyo ambaye amekuwa katika uhasama mkali na Kiduku kwa muda mrefu licha ya kuwa wawili hao hawajawahi kupanda ulingoni kuzichapa.

Kiduku amepata ushindi huo ikiwa ni miezi mitano imepita tangu alipopigwa na Asemahle Wellem kutoka Afrika Kusini na kuelekea pambano hilo alijitamba kuwa ataingia kama nyoka aliyekanyagwa mkia.

Kupitia kauli hiyo ndipo kulipomuibua Mwakinyo ambaye katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram, ameandika ujumbe uliosomeka kuwa:"Ni nyoka mwenye mapengo pekee akikanyagwa mkia ndio hurusha mate matupu".

Tags: