Simba SC yaishusha Azam FC kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara

© Kwa Hisani

KANDANDA Simba SC yaishusha Azam FC kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara

Zahoro Mlanzi • 20:00 - 05.10.2023

Simba SC wapanda kileleni Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons. Clatous Chama, John Bocco, na Saido Ntibazonkiza wafunga.

Timu ya Simba SC, imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Tanzania Prisons.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, umeifanya Simba kufikisha alama 12 ikiishusha Azam FC yenye alama 10 huku watani zao wa jadi, Yanga ikiwa katika nafasi ya tatu kwa alama 9.

Mabao ya Simba katika mchezo huo, yamefungwa na Clatous Chama, John Bocco na Saido Ntibazonkiza kwa mkwaju wa penalti huku bao pekee la Prisons likifungwa na Edwin Balua.

Simba ambayo kwa siku za hivi karibuni imekuwa ikikosolewa kutokuwa na kandanda safi licha ya kupata matokeo, imeonesha utofauti ukilinganisha na michezo mitatu iliyopita kwa kucheza soka la pasi fupi fupi kwenda mbele na kutoa burudani kwa mashabiki wao.

Licha ya uwanja huo kuonekana kama kuwa mkavu, lakini wachezaji wa Simba wamekuwa watulivu katika upigaji pasi zao na zikawa zinawafikiwa vizuri walengwa.

Prisons yenyewe imecheza soka la kushambulia kwa kushtukiza ikitumia mipira mirefu zaidi na ikajikuta ikinufaika kwa kufunga bao dakika 12 kupitia kwa Balua.

Umepigwa mpira mrefu ambao ulizaa faulo iliyopigwa na Balua na kwenda moja kwa moja wavuni huku Kipa, Ally Katoro akiruka bila mafanikio.

Dakika ya 32, Chama ameisawazishia Simba akiitendea haki pasi ya Kapombe na katika dakika 2 za nyongeza za kipindi cha kwanza, Bocco amewainua mashabiki wao kwa kufunga bao la pili akiunganisha pasi ya Mzamiru Yassin.

Zikiwa zimebaki dakika saba kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, Ntibazonkiza amefunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti baada ya Mosses Phiri aliyeingia badala ya Bocco kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari na Kipa, Yona Amos ambapo Mwamuzi Ester Aderbet ameamuru ipigwe penalti.