Kipre Jr. apiga 'hat trick' Azam ikishinda 5-0

LIGI KUU Kipre Jr. apiga 'hat trick' Azam ikishinda 5-0

Na Zahoro Mlanzi • 21:30 - 24.11.2023

Nyota huyo anaungana na Baleke, Aziz KI na Fei Toto kufunga idadi hiyo ya mabao msimu huu katika ligi hiyo

Winga Kipre Junior, ameifungia mabao matatu 'hat trick' timu yake ya Azam FC katika ushindi wa mabao 5-0 walioupata dhidi ya Mtibwa Sugar katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Ushindi huo, umeifanya Azam kufikisha alama 23 na kujichimbia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na Yanga SC yenye alama 24 na Simba SC ikibaki nafasi ya tatu kwa alama 19.

Huo ni ushindi wa wa tatu mfululizo kwa Azam tangu ilipofungwa na Namungo FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mbali na Kipre Jr kufunga mabao hayo pekee yake, mengine katika mchezo huo yalifungwa na Lusajo Mwaikenda kwa kichwa akiunganisha krosi ya Feisal Salum na baadaye Feisal alifunga la Tano.

Kipre Jr. anaungana na Jean Baleke wa Simba, Stephane Aziz KI wa Yanga na Feisal wa Azam kuwa wachezaji pekee waliofunga hat trick katika ligi hiyo.

Mchezo huo ambao haukuwa na mashabiki wengi, Azam ilitawala katika kila kipindi.

Ndani ya dakika ya 45 za kwanza, Kipre Jr alionekana kuwa nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao mawili katika dakika za 29 na 43.

Kipindi cha pili, Azam iliendelea kuliandama lango la Mtibwa na dakika ya 61, Mwaikenda alifunga bao la tatu kwa kichwa.

Zikapita dakika mbili tangu kufungwa kwa bao la tatu, Kipre akafunga bao la nne baada ya kufanya jitihada binafsi kwa kukimbia na mpira kutoka nyuma hadi kwenda kufunga kwa shuti kali lililomshinda kudaka Kipa, Mohamed Makaka.

Mashabiki wachache walionekana kuwepo uwanjani hapo wakiamini hakutafungwa mabao zaidi, zikiwa zimebaki dakika 3, Feisal alifunga bao la tano akimalizia mpira uliotemwa na Makaka kutokana na shuti lililopigwa na Idd Seleman 'Nado'.

Baada ya ushindi huo, Azam sasa inajiandaa na mchezo wao dhidi ya KMC utakaopigwa Desemba 8 kwenye uwanja huo huo.

Tags: