Manula kuikosa Asec Mimosa michuano ya Afrika

KANDANDA Manula kuikosa Asec Mimosa michuano ya Afrika

Na Zahoro Mlanzi • 20:00 - 24.11.2023

Kipa huyo ameumia tena ikiwa ni wiki chache tangu atoke majeruhi aliyokaa kwa zaidi ya miezi saba

Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Simba SC, Daniel Cadena, amesema atamkosa Kipa wake, Aishi Manula katika mchezo wa kesho dhidi ya Asec Mimosa kutokana na majeraha.

Simba itashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kukabiliana na Mimosa kwenye mchezo wa kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Cadena amesema Manula ana jeraha kwenye mguu wake na hivyo si sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kesho.

"Ni kweli Manula ametoka kwenye majeraha lakini hata mechi ya kesho hatakuwa kwenye kikosi kwasababu ana maumivu kwenye mguu," amesema.

Manula msimu huu hajaichezea mechi yoyote timu yake kutokana na kuwa majeruhi tangu Aprili ambapo alifanyiwa upasuaji wa nyama za paja nchini Afrika Kusini.

Mwezi uliopita ndio amerejea uwanjani na kuanza kufanya mazoezi mepesi kabla ya kuungana na timu yake kuendelea na programu kamili ya timu.

Baada ya kuonesha maendeleo mazuri, alirejeshwa katika kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' katika mechi za kujiandaa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Niger na Morocco na alifanikiwa kudaka katika mechi dhidi ya Niger ambapo Stars ilishinda 1-0.

Mbali na Manula kocha huyo, pia amesema wachezaji wengine wote wapo kamili lakini Cloutas Chama alichelewa kujiunga na timu akitokea kwenye timu yake ya Taifa ya Zambia hivyo wanajipa muda wa kumuangalia zaidi.

Tags: