Kiduku apania kumtwanga Mganda Sebyala Desemba 26

NGUMI Kiduku apania kumtwanga Mganda Sebyala Desemba 26

Zahoro Mlanzi • 14:32 - 04.12.2023

Bondia huyo mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Julai 29 dhidi ya Asemahle Wellem raia wa Afrika Kusini na alipoteza kwa pointi

Bondia wa uzito wa kilo 76 'Super middleweight' nchini Tanzania, Twaha Kiduku, amesema hatowangusha mashabiki zake wakati akipigana na Mohamed Sebyala kutoka Uganda.

Pambano hilo ambalo ubingwa wake bado haujawekwa hadharani na waandaaji Kampuni ya Peak Time, linatarajia kufanyika Desemba 26 kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Akizungumza na Pulsesports kuhusu maandalizi yake kuelekea pambano hilo, Kiduku amesema anajua aliwaangusha mashabiki zake katika pambano la mwisho lakini muda aliokaa bila kupanda uliongoni ameutumia vizuri kujiandaa kwa ajili ya mapambano yanayofuata kwa kuanzia na hilo.

"Katika pambano langu la mwisho nilipigwa hapa nyumbani mbele ya mashabiki wangu, kweli nakiri nilifanya makosa lakini siwezi kurudia katika pambano hili la ubingwa," amesema Kiduku.

Mara ya mwisho Kiduku anapanda ulingoni ilikuwa ni Julai 29 kwenye pambano ambalo sio la ubingwa na alipoteza mbele ya Asemahle Wellem raia wa Afrika Kusini ambaye alishinda kwa pointi.

Mbali na pambano la Kiduku lakini pia kutakuwa na mapambano 10 ya utangulizi.

Katika mapambano hayo ya utangulizi patashika itakuwa kwenye pambano baina ya Said Bwanga ambaye atakabiliana na Francis Miyeyusho.

Tags: