Taifa Stars yapiga tizi mara mbili Ivory Coast
Kocha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Adel Amrouche, amesema wanaendelea vizuri na maandalizi yao kuelekea michuano ya Afcon nchini Ivory Coast huku wakiwa na ratiba ya mazoezi mara mbili kwa siku.
Akizungumza akiwa nchini humo, Amrouche amesema tangu walipofika Jumatatu kikosi kimekuwa kikiendelea na ratiba walizopanga na amefurahi kuona wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri ya kiushindani.
"Tunaendelea vizuri na ratiba zetu kama tulivyopanga, tuna ratiba ya kufanya mazoezi mara mbili kwa siku na ninafuraha kuona wachezaji wakiwa bado katika hali nzuri," amesema.
Stars wamefikia katika Mji wa San Pedro ambapo watacheza michezo yao mitatu ya hatua ya makundi dhidi ya Morocco, Zambia na DR Congo.
Maandalizi ya Stars yalianza tangu wakiwa Tanzania ambapo waliweka kambi fupi visiwani Zanzibar kabla ya kurejea Dar es Salaam na kwenda Misri ambapo walikaa kwa wiki moja.
Kikosi hicho kilihitimisha kambi ya Misri kwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Misri ambapo walikubali kichapo cha mabao 2-0 siku ya Jumapili.