Rais Singida FG aweka wazi sababu kuwaacha Rupia, Onyango

Rais wa timu ya Singida FG, Japhet Makau, akizungumza

KANDANDA Rais Singida FG aweka wazi sababu kuwaacha Rupia, Onyango

Na Zahoro Juma • 19:23 - 26.01.2024

Klabu hiyo imeachana na nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza wa ndani ma hata wale wa kimataifa kitu ambacho si kawaida

Hatimaye uongozi wa timu ya Singida Fountain Gate, umeweka wazi sababu kubwa ya kufanya biashara ya kuwauza wachezaji wao nyota waliokuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza ni kupata fedha za kulipa madeni.

Timu hiyo mara baada ya michuano ya Mapinduzi Cup msimu huu, iliuza nyota wake zaidi ya 10 wakiwemo wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali.

Baadhi yao ni Wakenya, Elvis Rupia ambaye aliibuka Mfungaji Bora katika Mapinduzi Cup, Joash Onyango na Duke Abuya, Morice Chukwu, Mukrim Issa, Khomeiny Khomeiny, Marouf Tchakei na Meddie Kagere huku Mtanzania Gadiel Michael akiuzwa Cape Town City ya Afrika Kusini.

Timu hiyo kwa sasa ipo ndani ya tano bora na imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kutokana na mipango iliyokuwa nayo kwenye kusaka ushindi.

Akizungumza na Pulsesports, Rais wa Singida Fountain Gate, Joseph Makau, amesema wanatambua umuhimu wa kuwa na wachezaji wazuri na walifanya biashara na timu ili kupata fedha kwa ajili ya kulipa madeni.

“Ni kweli tumeuza baadhi ya wachezaji wetu ili kupata fedha za kulipa madeni ya klabu. Kuna timu ambazo zilikuja kwa ajili ya kupata wachezaji wetu tulikaa nao mezani na tulishindwana kwenye bei,” amesema.

Uamuzi huo wa Singida FG ulipokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa soka nchini Tanzania kwani haikuwekwa wazi sababu ya kuachana na nyota wao wengi tegemezi.

Tags: