FIFA yairuhusu Yanga kusajili wachezaji wapya

KANDANDA FIFA yairuhusu Yanga kusajili wachezaji wapya

Na Zahoro Mlanzi • 15:34 - 13.12.2023

Timu hiyo ilipewa siku 45 na FIFA kulipa deni la kiungo wao wa zamani, Gael Bigirimana ambaye walimvunjia mkataba bila kumpa stahiki zake

Wakati dirisha dogo la usajili la Tanzania Bara likitarajiwa kufunguliwa Ijumaa, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), limeifungulia timu ya Yanga SC, kufanya usajili baada ya kulipa deni walilokuwa wakidaiwa na kiungo wao wa zamani, Gael Bigirimana.

Yanga ilimsajili kiungo huyo kwa mkataba wa miaka miwili lakini alihudumu ndani ya mwaka mmoja baada ya kutovutiwa na kiwango chake na kuvunja mkataba naye.

Nyota huyo baada ya kusumbuliwa kupata haki yake aliamua kufungua kesi ya madai FIFA na hatimaye kushinda ndipo ilipoamuriwa Yanga kufungiwa kusajili ndani na nje hadi itakapolipa deni hilo ndani ya siku 45.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), FIFA imeiondolea adhabu hiyo Yanga baada ya kukamilisha malipo hayo.

Baada ya kukamilisha malipo hayo, TFF pia imeifungulia Yanga iendelee kusajili usajili wa ndani.

Akizungumza na Pulse Sports baada ya kutolewa taarifa hiyo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema suala la usajili kwao ni muhimu na ndio maana kuelekea kufunguliwa kwa dirisha hawakutaka kuwa na kizuizi chochote.

Ameongeza taarifa ya kocha imebainisha baadhi ya nafasi ambazo zinatakiwa kuboreshwa katika dirisha hili na uongozi unaendelea kufanyia kazi ili kuweza kupata mafanikio makubwa mwisho wa msimu huu.

"Sisi suala la usajili kwetu ni muhimu na ndio maana tumeona ni vyema tukajisafisha kabla ya dirisha kufunguliwa, uongozi wa juu ulishapokea taarifa ya kocha na sasa wapo bize wanafanyia kazi ili kutekeleza kile ambacho kinahitajika," amesema.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, Yanga imekuwa ikihusishwa kutaka kufanya usajili wa winga wa Mtibwa Sugar, Ladaki Chasambi, nyota wa timu ya Taifa ya Ghana na SC, Jonathan Sowah, pamoja na mshambuliaji raia wa Cameroon, Lionel Ateba kutoka katika Klabu ya Dynamo of Douala.