Mwakinyo sasa kuzichapa na Mkongo Nkanku Januari 27

NGUMI Mwakinyo sasa kuzichapa na Mkongo Nkanku Januari 27

Na Zahoro Mlanzi • 09:00 - 08.01.2024

Pambano hilo ni la kuwania ubingwa wa mkanda wa WBO Afrika ambalo litafanyikia visiwani Zanzibar

Bondia wa Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo, amebadilishiwa mpinzani katika pambano lake la kuwania ubingwa wa WBO Afrika na sasa atazichapa na Mkongo, Mbiya Nkanku badala ya Mzimbabwe, Enock Msambudzi.

Pambano hilo linatarajiwa kufanyika Januari 27 katika Ukumbi wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoiweka katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Mwakinyo, pambano hilo litakuwa la uzito wa kilogramu 72 na litapigwa kwa raundi 10.

Taarifa hiyo ya Mwakinyo imekuja ikiwa zimepita siku kadhaa tangu kutangazwa kwa pambano hilo la awali.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari mbalimbali, mpinzani wa awali wa Mwakinyo alikuwa hana sifa za kuwania mkanda huo na ndio maana waandaji wa pambano hilo wakaamua kubadilisha mpinzani mara moja.

"Nasikitika Januari 27 sitaweza kucheza na Msambudzi kwasababu ya taratibu za wasimamizi wa ngumi duniani ingawa nilimpania sana," amesema Mwakinyo kupitia mtandao wake wa Instagram.

Nkanku sio jina geni kwa wapenzi wa ngumi nchini kwani mwaka 2016 aliwahi kucheza dhidi ya bondia, Twaha Kiduku na akapigwa kwa KO katika raundi ya 6 pambano ambalo lilifanyika Lusaka, Zambia.

Hilo litakuwa ni pambano la kwanza kwa Mwakinyo tangu lilipotokea sakata lake la kugoma kupanda ulingoni Septemba, mwaka jana kuzichapa na Julius Indongo na kisha kufungiwa kabla ya kufunguliwa mwezi uliopita na  Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC).

Mara ya mwisho Mwakinyo kupanda ulingoni ilikuwa Aprili, mwaka jana ambapo alipigana Dodoma dhidi ya Mardochee Kuvesa Katembo.