Bondia wa Ngumi za Kulipwa wa Tanzania, Abdallah Pazi 'Dullah Mbabe', amesema maandalizi yake kuelekea pambano la Novemba 25 dhidi ya Tshimanga Katompa yapo vizuri na ana uhakika wa kufanya vizuri.
Pambano hilo linatarajia kufanyika jijini Arusha kwenye Ukumbi wa AICC huku Kampuni ya Lad in Red Promotion wakiwa ndio waandaaji.
Dullah ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Pulsesports akiwa katika maandalizi makali kabla ya kuvaana na Katompa ambaye ni raia wa DR Congo.
"Ninajiamini na maandalizi yangu, kambi yangu ipo hapa Dar es salaam, na hivi karibuni nitakwenda Arusha, nina maandalizi mazuri ambayo nina uhakika yatanipa ushindi," amesema.
Pambano hilo ambalo sio la ubingwa litakuwa ni la raundi 10, litawakutanisha mabondia hao wenye nia tofauti ambapo Dullah Mbabe anataka kulipa kisasi na Katompa kuendeleza ubabe.
Ikumbukwe mwaka 2021, wawili hao walipanda ulingoni na Katompa aliibuka na ushindi wa pointi dhidi ya Dullah.
Pambano la marudiano ambalo lilipangwa kufanyika mapema mwaka huu halikufanikiwa baada ya Katompa kuingia mitini hivyo kwa kipindi hiki ni wazi wawili hao watakutana jijini Arusha.