Rupia, Abuya waing'arisha Ihefu FC ikiichapa Mtibwa 3-2

KANDANDA Rupia, Abuya waing'arisha Ihefu FC ikiichapa Mtibwa 3-2

Na Zahoro Juma • 17:03 - 12.02.2024

Nyota hao waliachwa na Singida FG katika dirisha dogo na kusajiliwa na timu hiyo

Kikosi kilichojaa sura mpya cha Ihefu FC ya Mbeya, kimeanza kwa kutamba ugenini baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika katika Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Bao la ushindi kwa Ihefu lilifungwa na mshambuliaji Mkenya, Elvis Rupia ambaye alianza ligi akiwa na klabu ya Singida FG.

Rupia ambaye aling'ara na Singida FG kwa kuibuka Mfungaji Bora katika michuano ya Mapinduzi Cup, akitupia mabao matano.

Katika mchezo huo, Ihefu ilitangulia kwa mabao mawili ambayo yalifungwa na Mkenya, Duke Abuya na Maoruf Tchakei.

Hata hivyo, Mtibwa Sugar ilirejea mchezoni kwa kuchomoa mabao hayo kupitia kwa Kassim Shaban na Juma Luizio.

Baadhi ya nyota wengine wapya ambao walicheza kwa upande wa Ihefu wakiwa ni usajili wa dirisha dogo ni Morice Chukwu, Joash Onyango na Khomeini Abuubakar.

Kwa matokeo hayo, Ihefu imefikisha alama 16 na wamepanda hadi nafasi ya 12 huku Mtibwa Sugar wakisalia mkiani wakiwa na alama zao nane.

Tags: