Kagera Sugar yamtimua Kocha wao Mexime

BREAKING NEWS Kagera Sugar yamtimua Kocha wao Mexime

Na Zahoro Mlanzi • 18:20 - 22.12.2023

Timu hiyo imefikia uamuzi huo ikiwa ni siku moja imepita tangu ipoteze mechi yao kwa kufungwa 4-0 na Azam FC

Uongozi wa Klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kager, umefikia uamuzi wa kumfuta kazi Kocha, Meck Mexime ikiwa ni siku moja tu baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Kagera Sugar kuwa na mwendo wa kusuasua kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara ikiwa wameshuka dimbani mara 13 na kukusanya alama 13.

Mexime alijiunga na Kagera Sugar katikati ya msimu uliopita kuchukuwa nafasi ya Kocha. Mkenya, Francis Baraza.

Mbali na Mexime lakini pia Kagera Sugar wametangaza kuachana na Kocha wao wa Viungo, Francis Mkanula.

"Tumefikia maamuzi ya kuachana na Kocha Mkuu, Mecky Mexime, vile vile tumeachana na Kocha wa Viungo Francis Mkanula," imesomeka taarifa ya Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa Kagera kikosi cha timu hiyo kitakuwa chini ya Kocha wa mpito, Marwa Chamberi ambaye ataongoza timu wakati zoezi la kusaka kocha mpya likiendelea.

Mchezo unaokuja wa Kagera katika ligi watawaalika Yanga, Desemba 26 katika Uwanja wa Kaitaba lakini mchezo huo umeahirishwa.

Mexime anatimiza idadi ya makocha 12 waliotimuliwa na timu mbalimbali msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara.

Tags: